Data Loading...

KUTUNZA UKE Flipbook PDF

KUTUNZA UKE


122 Views
26 Downloads
FLIP PDF 94.98KB

DOWNLOAD FLIP

REPORT DMCA

Ujue Uke Wako Watu huwa na maumbo, rangi na saizi na tofauti. Hata uke pia huwa unatofautiana kati ya mwanamke mmoja na mwingine. Pia uke wako unaweza kuwa tofauti kulingana na umri wako. Ulivyokuwa mtoto, ulipobalehe, ulipokuwa msichana na hata kabla na baada ya kuzaa uke wako unabadilika badilika na utaendelea kubadilika. (PICHA) Sehemu ya nje ya uke Ukiangalia sehemu zako za siri utaona kuna matundu mawili. Tundu moja ni la uke na tundu lingine ni la mkojo. Viungo vyote unavyoviona kwa nje vinavyozunguka hayo matundu mawili, vinatengeneza sehemu ya nje ya uke. Viungo hivyo ni kinena, labia kubwa, labia ndogo, kisimi na msamba. Wataalamu huwa wanaita hivi viungo vulva. (PICHA) Kinena Kinena ni sehemu nene yenye mafuta na umbo la nusu mviringo iliyofunikwa na nywele. Jukumu la tishu ya mafuta kwenye kinena ni kulinda eneo la kinena la mwanamke lisiumie anapofanya tendo la ndoa. Labia kubwa na labia ndogo Labia kubwa ni mapindo mawili marefu ya ngozi yenye mafuta na yaliyofunikwa na nywele. Mapindo haya hufunika na kulinda viungo vingine vyaa Sehemu ya siri.

Labia ndogo ni mapindo mawili madogo ya tishu yaliyofunikwa na labia kubwa. Hulinda mwanya wa uke na urethra. Labia ndogo kwa kawaida ni nyumbulifu kiasili, sifa inayozifanya ziweze kutanuka na kunywea wakati wa ngono, wakati wa leba na hata wakati wa kuzaa. Labia huwa katika rangi tofauti tofauti, kuanzia pink au zambarau, kahawia na hata nyeusi. Kwa wanawake weusi, mara nyingi labia ni nyeusi zaidi kuliko sehemu nyingine za mwili wa binadamu.Labia inaweza kupauka kadiri unavyozeeka, au kuwa nyeusi zaidi pale unapokuwa umesisimka. Lakini iwapo itatokea na kubadilika rangi ghafla na kuwa nyekundu na kuvimba, inaweza kuwa ni dalili ya maambukizi. Umbo la labia inatofautiana sana kutoka kwa mwanamke mmoja na mwinginemtu. Baadhi ya maumbo ya kawaida ni pamoja na: Mashavu ya nje yanakuwa marefu: Labia ya nje inaweza kuwa ndefu au fupi. Wakati mwingine kwa baadhi ya wanawake, mashavu ya nje yanakuwa yamekutana na kuyaficha mashavu ya ndani. Mashavu ya ndani yanaweza kuwa marefu: Wakati mwingine, labia ya ndani hurefuka na kuvuka mashavu ya nje.

Mashavu ya ndani yanaweza kuwa wazi: Kwa baadhi ya wanawake, labia ya nje huwa ni fupi au imepinda, hivyo kufanya mashavu ya ndani yaonekane hata kama labia ya ndani si mirefu sana. Zinaweza zisilingane: Sio ajabu kwa mwanamke mmoja kukuta labia zake zinatofautiana.Unaweza kukuta upande mmoja wa labia ya ndani au ya nje unakuwa mrefu kuliko upande mwingine. Wanawake wengine wana labia kubwa na wengine ndogo. Na labia yako inaweza kubadilika na umri. Unapokaribia kukoma hedhi, mabadiliko ya homoni yanaweza kusababisha uke kusinyaa kidogo. Kisimi Kisimi ni viungo vifupi vyenye uwezo wa kuhusi. Viungo hivi vina neva na mishipa ya damu kwa wingi. Jukumu lake ni kumsisimua mtu wakati wa ngono na ni nyepesi sana kuhisi hasa kwa mguso. Mahali ilipo kianatomi ni sawa na mahali ulipo uume kwa mwanamume. Tundu la mkojo. Kazi yake ni kupitisha mkojo kwa nje kutoka kwenye kibofu cha mkojo. Tundu la uke Kazi yake ni kupitisha mtoto wakati wa kuzaa, kupitisha damu ya hedhi na kupitisha uume wakati wa tendo la ndoa.

Tofauti za uke Kama miundo ya nje ilivyo tofauti, ndivyo anatomy ya ndani ya wanawake pia inatofautiana. Urefu wa wastani wa uke (mrija wa kunyoosha) ni inchi 4, lakini inaweza kuwa ndefu au fupi, pana au nyembamba. Saizi haijalishi, kwa sababu kwa asili yake huwa una tanuka wakati wa ngono na wakati wa kujifungua. Msamba Eneo lenye misuli lililofunikwa na ngozi kati ya mwanya wa uke na mkundu huitwa msamba. Eneo hili lina misuli yenye nguvu na neva na husaidia kwa kuegemeza viungo vilivyo kwenye nyonga. Utanzaji wa Uke Uke haujitaji mambo mengi kama ambavyo baadhi ya wanawake wa kileo wamekuwa wakiamini. Kwa kiasi kikubwa, uke unahitaji huduma ya msingi tu ili kuufanya uwe wenye afya. Vifuatavyo ni vidokezo vya kukusaidia kutunza uke wako ili uwe wenye afya na wewe uwe mwenye furaha.

1. Usitawaze.

Kutawaza ni namna ambayo mwanamke huosha sehemu ya ndani ya uke kwa kutumia maji pekee au mchanganyiko wa maji na kemikali. Wanawake wengi wamezaliwa na kufundisha kwamba usafi wa mwanamke unahusisha kutawaza. Mazoea haya yamejengeka na kuwa kama miiko ambayo wanawake wengi ni lazima waifuate. Mwanamke anapoambia kwamba haupaswi kutawaza au kuingiza chochote ukeni anaona hii ni elimu gani tena. Kwanini wanawake wanatawaza Idadi kubwa ya Wanawake hutawaza kila siku. Ukiwauliza kwa kwanini wanatawaza watakuambia kutawaza kunasaidia kuondoa au kuzuia harufu mbaya, ama wanataka kuondoa damu za hedhi. Wengine watakuambia wanatawaza baada ya tendo la ndoa kama njia kuzuia mimba na wengine ili kuzuia kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa.Baadhi ya wanawake huamini kuwa kutawaza huwafanya kuwa safi. Lakini licha ya kwamba kutawazwa umefungwa na bibi au na shangazi wataalam wa afya pamoja na madaktari wa magonjwa ya wanawake hawapendekezi kutawaza.

Je kutawaza kuna faida ? Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa kutawaza hakuna faida isipokuwa kutawaza kuna husishwa na matatizo mengi ya kiafya kwa wanawake. Hasara za kutawaza Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa kutawaza kuna madhara mengi kuliko faida. Yafuatayo ni baadhi ya madhara yatokanayo na kutawaza:1.Maambukizi ya bakteria (Bacterial vaginosis) -Wanawake wanaotawaza wako kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi sehemu za siri 2.Maambukizi kwenye mfuko wa uzazi Kutawaza mara kwa mara inaongeza uwezekano kwa mwanamke kupata maambukizi kwenye mfuko wa uzazi 3.Kutawaza na mimba Wanawake wanaotawaza zaidi ya mara moja kwa wiki ni ngumu kupata mimba kuliko wenzao ambao hawafanyi hivyo.Pia tafiti zinaonyesha kwamba kutawaza kunaongeza hatari ya mimba kutunga nje ya mfuko. 4. Saratani ya shingo ya kizazi Baadhi ya tafiti zimebainisha kuwa kutawaza angalau mara moja kwa wiki kunaongeza hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi. Mwanamke afanye nini? Mwanamke anashauriwa kuosha sehemu ya nje tu ya uke. Mwanamke hashauriwi kuingiza kitu chochote hata kidole sehemu zake za siri. Kwa asili uke huwa unajisafisha wenyewe. Kwa hiyo hakuna haja ya kuosha ndani au kujitawaza kwa kuingiza vidole au kemikali zingine ukeni. Kutawaza kunaweza kusababisha mabadiliko yasiyofaa katika pH (asidi) na uwiano wa bakteria wa kawaida waa uke hali inayopelekea uwe unapata maambukizi ya bakteria ya mara kwa mara. 2. Weka msingi. Kula vizuri, pata usingizi wa kutosha, na ufanye mazoezi mara kwa mara ili kusaidia sehemu zote za mwili wako kuwa na afya.

3.

Shiriki ngono iliyo salama.

Jifunze historia ya ngono ya wenzi wako na ufanye ngono salama zaidi. Acha kushiriki ngono zembe madhara yake yanaweza kuwa makubwa kwenye afya ya uke wako. Kama utaingia katika mahusiano mapya tumia kondom kwa muda wa miezi 6. Unaweza kuacha kutumia kondomu baada ya wewe na mwenzi wako kupima mara mbili na kujiridhisha kwamba nyote ni waaminifu. Kutumia kondomu itakusaidia kukuepusha na magonjwa mengi ya ngono pamoja na mimba zisizotarajiwa. 4. Jiachie. Thongs zinaweza kusugua huku na huko, pia na chupi za kubana, spandex na chupi za kutengeneza zinaweza kuongeza joto na unyevunyevu na kusababisha miwasho. Vaa nguo zisizokuwa za kubana na chupi zilizotengenezwa kwa nyuzi asilia kama vile pamba. Kulala bila nguo ya ndani au kitu chochote kinachobana huruhusu hewa kufika kwenye eneo la uke na husaidia kufanya tishu za uke ziwe na afya. .

5. Weka safi. Ili kusaidia kuzuia kuenea kwa bakteria ambao wanaweza kusababisha maambukizi ya njia ya mkojo, kila baada ya kujisaidia haja kubwa jifute kutoka mbele kwenda nyuma. 6. Chukua tahadhari unapotumia tampon Kama unatumia tampons, zitumie kwa busara. Chagua zenye uwezo mkubwa wa kunyonya badilisha tampons kila baada ya masaa mawili hadi nane. Usilale na tampon usiku kucha. 7. Usizidishe. Ili kusafisha uke wako, Safisha kwa vidole vyako kwa kutumia maji ya vuguvugu tu na au sabuni isiyo kuwa kali au isiyo na manukato. Epuka kujiloweka kwa muda mrefu katika maji ya moto, ambayo yanaweza kusababisha uke wako kukauka na kusababisha kuwashwa. 8. Epuka vitu vinavyoweza kusababisha miwasho ukeni. Epuka sabuni zenye manukato, viondoa harufu mwilini na manukato. Hizi zinaweza kusababisha baadhi ya wanawake wapate miwasho. Iwapo una ngozi laini, tumia toilet paper nyeupe zisizokuwa na manukato, tumia sabuni ambayo haisababishi aleji na epuka fabric softener unapokausha nguo zako za ndani.

HARUFU YA UKE Harufu ya kawaida ya Ule Ikoje

Uke huwa una harufu yake wenyewe, kama vile zilivyo sehemu nyingine za mwili wako. Ni kawaida kwa uke kuwa na harufu nzuri ya kuvutia ((( tindikali ))) na, wakati wa hedhi uke huwa unakuwa na harufu ya metali. Ni kawaida kabisa uke kuwa na harufu tofauti kulingana na siku tofauti za mzunguko wa mwanamke. Pia mwanaume akimwagia ndani ya uke inaweza kusababisha harufu ya uke wako kubadilika kwa muda wa siku 1 au 2. Harufu isiyokuwa ya kawaida Ukeni Kwa kawaida kila mwanamke anatoa harufu ya kuvutia ukeni ambayo huwa haiwi kero kwa mwanamke mwenyewe au kwa mwenzi wako. Wakati mwingine baadhi ya wanawake huwa wanatoa harufu ya kukera kutoka ukeni.Iwapo unatoa harufu kali sana ukeni au harufu isiyokuwa ya kawaida, na mabadiliko hayo hayakuwepo inawezekana una maambukizi. Nenda hospitali umuone daktari na katika kipindi chote hicho epuka kujinunulia dawa au kushiriki tendo la ndoa mpaka utakapopata matibabu na kupona. Hizi ndio sababu zinazosababisha mwanamke kutoa harufu Harufu mbaya sio tu kwamba inakera bali pia inadhoofisha maisha ya mwanamke na kumfanya mwanamke aishi kwa hofu na hata kuvuruga mahusiano yake na mwenzi wake. Wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kubaini sababu ya harufu. Ziifuatazo ndio sababu ambazo mara nyingi huwa zinasababisha mwanamke kutoa harufu ukeni :1.Kitu kilichoshaulika sehemu za siri kama kondom au tampon - Harufu huwa mbaya kama mzoga 2. Bacterial Vaginosis (BV) Ugonjwa huu unasababisha mwanamke kutoa harufu mbaya kama shombo ya samaki hasa wakati wa tendo la ndoa 3.Trichomoniasis Huu ni ugonjwa wa zinaa, husababisha mwanamke kutoa harufu mbaya kama mayai yaliyooza 4.Fistula -Inaweza kutoa harufu ya mkojo au 5. Kansa 6. Kuvuja mkojo 7.Choo kubwa kuvuja 8. Maambukizi mengine 9. Uchafu wa mwili 10. Kuvuja jasho sana kunakoambatana na uzito mkubwa na unene Kama una toa harufu yoyote isiyokuwa ya kawaida ni muhimu kwenda hospital kwa uchunguzi zaidi kwa sababu baadhi ya magonjwa yanaweza kuhatarisha maisha yako au kuleta madhara katika mfumo wa uzazi. Katika sura ya mbele utajifunza kuhusu maambukizi.

UTE WA UKE Wanawake wote hutoa majimaji na ute kutoka kwenye kuta zinazozunguka uke na seviksi. Ute huu unaweza kuwa mweupe au kama na unaweza kuwa unateleza au kunata. Ute huo unapokauka unaweza kuwa na rangi ya manjano. Unaposisimka mfano wakati wa ngono au wakati wa stress au katikati ya mzunguko wako wa hedhi ute huwa unatoka kwa wingi. Ute wa kawaida hausababishi muwasho, maumivu au uke kuvimba. Iwapo ute unaotoka ukeni

unaambatana na harufu isiyo ya kawaida, miwasho, maumivu na kuvimba ukeni inawezekana una maambukizi na unahitaji kwenda hospitali ili kuangaliwa. Kwa kawaida bakteria wa aina nyingi huwa wanaishi kwenye uke wa mwanamke mwenye afya njema. Bakteria hao wanaitwa bakteria rafiki. Baadhi yao, haswa wanaoitwa lactobacilli, husaidia kuweka uke kuwa na afya, kudumisha pH ya asidi (chini ya 4.5), na kudhibiti ukuaji wa bakteria hatari. Iwapo kitu chochote kitavuruguka uwiano wa bakteria rafiki kwenye Uke mwanamke atakuwa kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi kutoka kwa vimelea vya aina mbalimbali.

Maambukizi Ukeni. Katika wakati fulani wa maisha unaweza kupata maambukizi ukeni. Maambukizi hayo yanaweza kusababishwa na magonjwa yanayoenezwa kwa njia ya ngono na yale yasiyokuwa ya ngono. Ni jukumu lako wewe mwenyewe na mwenzi wako kujilinda msipate maambukizi ya magonjwa ya ngono, na kama yakitokea utambue dalili zake, upate matibabu na uweze kujilinda usimuambukize mwenzi wako au yeye asikuambukize. Kuchelewa kupata matibabu ya magonjwa ya zinaa kunaweza kusababisha kupata maumivu, ulemavu, kusababisha ugumbu na hata madhara kwa mtoto wako iwapo utabeba mimba ukiwa na baadhi ya magonjwa ya zinaa. Iwapo umepata maambukizi ya magonjwa ya zinaa, dalili zake zinaweza kujumuisha dalili zifuatazo:• Muwasho • Kutokwa uchafu ukeni. • Kutoa harufu isiyokuwa ya kawaida kutoka ukeni au kwenye njia ya haja kubwa. Ni muhimu uzingatie rangi au harufu inayotoka kwa wakati huo • Uvimbe, malengelenge, vidonda, au vipele, mara nyingi karibu na sehemu za siri au kwenye njia ya haja kubwa. • Maumivu makali chini ya kitovu. • Maumivu au kuchomachoma wakati wa kukojoa. • Maumivu wakati wa kujamiiana • Hedhi isiyokuwa na mpangilio Kutokwa damu wakati au baada ya kujamiiana. Magonjwa Yanayosababisha Vidonda/Vipele Sehemu za siri. Katika maeneo mengi magonjwa ambayo huwa yanasababisha vidonda au vipele sehemu za siri ni magonjwa ya Kaswende, Malengelenge na Ugonjwa wa Pangusa. Magonjwa haya yanaweza kusababisha kupata vidonda ukeni, kwenye njia ya haja kubwa na hata sehemu nyingine za mwili. Wakati mwingine mgonjwa anaweza kuwa maambukizi ya magonjwa yote kwa pamoja. Mara nyingi ni vigumu daktari kutambua ugonjwa kwa kusikiliza historia ya mgonjwa pekee na kwa kumuangalia. Kwa hiyo, ni muhimu watu wote ambao wana vidonda au vipele sehemu za siri, kwenye njia ya haja kubwa au msamba kufanyiwa uchunguzi. Magonjwa yanayosababisha kutoka uchafu ukeni

Hali ya mwanamke kutoka uchafu ukeni inaweza kusababishwa na magonjwa ya kuambukizwa na yasiyo ya kuambukizwa. Iwapo dalili zipo zinaweza kujumuisha kusikia maumivu wakati wa kukojoa, miwasho ukeni na kwenye tundu la mkojo pamoja na kutoka usaha au majimaji. Baadhi ya wagonjwa wanaweza kuwa wanatoka uchafu bila dalili nyingine zozote. Mara nyingi magonjwa ya kisonono, Klamidia na TRICHOMONIASIS ndio huwa yanasababisha mtu kutoka uchafu ukeni au kwenye tundu la mkojo. Wagonjwa wenye maambukizi haya ni vizuri kufanyiwa uchunguzi wa kujua ni maambukizi ya namna gani ili kuzuia maambukizi zaidi, madhara na kutoa matibabu sahihi. Magonjwa Yanayosababisha Kuwashwa, Kuwaka moto ngua, Harufu, au Kutokwa uchafu ukeni. Idadi kubwa ya wanawake huwa wanakuwa na maambukizi ukeni ambayo huwa yanasababisha kutokwa na uchafu, kuwasha, maumivu kama unawaka moto, au harufu wakati fulani katika maisha yao. Mara nyingi wanawake wenye dalili hizi huwa wanajitibu kama fangasi wenyewe kwa kutumia dawa za tiba mbadala, virutubisho na dawa za hospitali kabla na hata baada ya kuonana na daktari. Haitoshi kwa daktari kusikiliza maelezo ya mgonjwa pekee kufanya utambuzi sahihi wa magonjwa haya na inaweza kusababisha mgonjwa kupewa dawa ambazo sio sahihi kwake.Kwa hiyo, ni muhimu daktari kupata maelezo mazuri kutoka kwa mgonjwa, kumfanyia uchunguzi wa mwili na kufanya vipimo maabara ili kubaini ni maambukizi ya aina gani. Daktari anaweza kukuhoji zaidi juu ya aina ipi ya ngono huwa unashiriki, hedhi yako, usafi wa uke (kama una tawaza) na kama umejitibia kwa dawa za kupaka ama kuingiza ukeni. Mara nyingi maambukizi ambayo huwa yanasababisha muwasho na kutoka uchafu ukeni ni pamoja na Maambukizi ya bakteria ukeni, Maambukizi ya Fangasi na TRICHOMONIASIS. Maambukizi ya Fangasi ukeni sio ugonjwa wa ngono lakini mara nyingi huwa yanapatikana wakati wa uchunguzi wa magonjwa mengine ya ngono.

KLAMIDIA Klamidia husababishwa na bakteria aina ya Chlamydia trachomatis. Unapataje maambukizi Unaweza kupata maambukizi ya ugonjwa wa Klamidia kwa aina zote za ngono. Iwapo kuna majimaji kwenye vidole, ukishika machoni utapata pia maambukizi machoni. Iwapo utashiriki ngono kwa njia ya mdomo unaweza kupata maambukizi kwenye koo. Wakati wa kujifungua, mama mwenye ugonjwa huu anaweza kumuambukiza mtoto. Klamidia ndio mara nyingi husababisha nimonia na macho mekundu kwa watoto wachanga. Dalili Mara nyingi idadi kubwa ya wanawake wenye ugonjwa huu huwa hawana za wazi. Maambukizi huwa yanaanzia kwenye mlango wa kizazi na kwenye tundu la mkojo (urethra). Kutoka uchafu usiokuwa ukeni na kusikia maumivu kama unaungua zinaweza kuwa dalili kwa baadhi ya wanawake wenye maambukizi. Iwapo mgonjwa asipopata matibabu, maambukizi yanaweza kusambaa na kutoka kwenye mlango wa kizazi hadi kwenye mirija ya

falopia. Hata baada ya maambukizi kufika huko baadhi ya wanawake wanaweza wasiwe na dalili zozote; wengine wanaweza kuwa na maumivu chini ya tumbo, kichefuchefu, homa, maumivu wakati wa kujamiiana, au kutoka damu kipindi kisichokuwa cha hedhi. Kwa Dalili za wanaume ni pamoja na kutokwa na uume au hisia inayowaka wakati wa kukojoa. Wanaume wanaweza pia kuwa na moto na kuwasha karibu na ufunguzi wa uume. Matibabu Iwapo utakuwa na maambukizi ya Klamidia daktari atakuanzishia antibiotiki. Ili kuepuka kuambukizwa tena ugonjwa huu hakikisha mwenzako naye anatibiwa. Baada ya miezi mitatu ni vizuri ukarudi hospitali ili kuchunguzwa tena. Matatizo Ugonjwa wa Klamidia unaweza kusambaa hadi kwenye mfuko wa uzazi au mirija ya uzazi na kusababisha ugonjwa ambao wataalamu wanaita PID. PID inaweza kusababisha majipu yaliyojaa usaha ndani maumivu ya muda mrefu ya nyonga. PID inaweza kuharibu mirija ya uzazi kiasi cha kusababisha ugumba au kuongeza hatari ya mimba kutunga nje ya kizazi. Chlamydia pia inaongeza hatari ya kupata maambukizi ya VVU

Ugonjwa wa Kisonono Ugonjwa wa Kisonono unasababishwa na maambukizi ya bakteria wanaojulikana kama Neiseria gonorrhoea. Unapataje maambukizi Kisonono huenezwa kwa kugusana na uume, uke, mdomo, au njia ya haja kubwa kutoka kwa mtu mwenye maambukizi. Mtoto anaweza kupata maambukizi ya Kisonono kutoka kwa mama yake wakati wa kujifungua. Kwa mtoto, ugonjwa huu unaweza kusababisha upofu, maambukizi ya viungo, kusambaa kwenye damu na hata kusababisha mtoto kupoteza maisha. Dalili Idadi kubwa ya wanawake ambao huwa na maambukizi mara nyingi huwa hawana dalili za wazi. Kwa wale wanaokuwa na dalili, zinaweza kuwa ni pamoja na kutoka usaha Ukeni,kuhisi maumivu wakati wa kukojoa na hedhi kuvurugika. Mara nyingi watu wengi wanaweza kufananisha dalili hizi na maambukizi kwenye njia ya mkojo.Kwa wanaume dalili zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kusikia maumivu wakati ya kukojoa na kutoka usaha kwenye uume, ambao unaweza kuwa na rangi nyeupe, ya njano au ya kijani. Maambukizi haya kwa wanaume pia yanaweza kusababisha korodani kuvimba na kuuma. Matibabu. Ugonjwa huu unaweza kutibiwa kwa antibiotiki. Hata hivyo matukio ya usugu wa dawa dhidi ya vimelea vya ugonjwa huu yameripotiwa katika maeneo mbalimbali. Wewe pamoja na mwenzi wako ni muhimu wote mpate matibabu. Rudi hospitali baada ya miezi 3 ili kufanyiwa uchunguzi hata kama hauna dalili.

Kisonono pamoja na Klamidia ndio sababu kubwa ya ugonjwa wa PID. Ugonjwa wa PID usipotibiwa unaweza kusababisha ugumba. UGONJWA WA KASWENDE Ugonjwa wa Kaswende unasababishwa na bakteria wanaoitwa Treponema pallidum. Unapataje maambukizi Ugonjwa wa Kaswende unaambukizwa kwa kugusana moja kwa moja na kidonda kutoka kwa mtu mwenye maambukizi. Mara nyingi vidonda hujitokeza sehemu za siri, kwenye uke au kwenye njia ya haja kubwa. Hata hivyo unaweza kupata kidonda cha ugonjwa wa Kaswende kwenye sehemu yoyote ya mwili hata kwenye vidole, mdomoni na kwenye ngozi. Kwa kawaida wanawake wote wajawazito huwa wanafanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa Kaswende kwa sababu mtoto anaweza kupata maambukizi ya ugonjwa huu akiwa bado tumboni kwa mama yake. Mama asipopata matibabu anaweza kuzaa mtoto mwenye ulemavu. Dalili zake Kwa kawaida ugonjwa wa Kaswende unapitia hatua tofauti tofauti kulingana na mgonjwa anavyochelewa kupata matibabu. Katika hatua ya awali Kaswende huwa inasababisha kidonda sehemu ya mwili ambapo bakteria waliingilia mwilini. Mara nyingi kidonda hiki huwa hakina maumivu. Baada ya muda kidonda hicho hupona chenyewe hata kama mgonjwa hakupata matibabu, lakini bado mgonjwa anakuwa na uwezo wa kuambukiza. Iwapo mgonjwa hakutibiwa, ugonjwa unaingia katika hatua ya pili. Mara huwa ni kuanzia wiki 2 hadi 8 baada ya kuwa ameona kidonda. Katika hatua hii bakteria huwa wanasambaa kwenye damu. Katika hatua ya pili mgonjwa huwa anakuwa na vipele kwenye mwili. Vipele hivi vinaweza kuonekana kama mabaka yenye rangi nyekundu au kahawia. Mabaka hayo yanaweza kuwa sehemu mbalimbali za mwili kuanzia kwenye viganja vya mkono na miguu, kwenye ngozi. Pia mgonjwa anaweza kuwa na vidonda kwenye sehemu laini za mwili, homa na kuvimba mitoki, maumivu ya kichwa, nywele kunyonyoka na dalili nyingine. Iwapo mgonjwa hakutibiwa katika hatua hii ugonjwa unaingia hatua ya tatu ambayo inaweza kuleta madhara kwenye mishipa mikubwa ya damu na kwenye ubongo. Uchunguzi Daktari anaweza kugundua kama una ugonjwa wa Kaswende kwa kuangalia dalili. Hata hivyo kuna vipimo vya maabara ambavyo unaweza kufanyiwa ili kuthibitisha kama una Ugonjwa wa Kaswende. Kwa kawaida wanawake wajawazito wote huwa wanafanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa Kaswende.

Matibabu Katika hatua za awali ni rahisi sana ugonjwa wa Kaswende kutibiwa. Katika hatua hiyo mgonjwa anahitaji dozi moja tu antibiotiki kutibiwa na kupona kabisa. Iwapo mgonjwa amekaa na ugonjwa kwa muda mrefu anahitaji kutumia antibiotiki kwa muda mrefu ili kupona. Katika kipindi chote cha matibabu epuka kushiriki ngono mpaka utakapopona kabisa. Ni muhimu mwenzi wako na yeye kupatiwa matibabu.

Madhara ya Kaswende ambayo haikutibiwa Iwapo ugonjwa wa Kaswende hakutibiwa utaingia katika hatua nyingine, ambako mgonjwa anaweza asionyeshe dalili zozote lakini ugonjwa unakuwa unamshambulia kimyakimya. Katika hatua ya mwisho ugonjwa huu huwa unasababisha uharibifu mkubwa katika viungo mbalimbali vya mwili ambavyo ni pamoja na moyo, macho, mishipa ya fahamu, ubongo, mishipa ya damu, ini, na viungo vingine vya mwili. Madhara yake yanaweza kusababisha mtu kupooza, upofu, ugonjwa wa akili au kupoteza maisha.

Ugonjwa wa TRICHOMONIASIS. Ugonjwa huu ndio unaoathiri idadi kubwa ya wanawake. Unasababishwa na vimelea aina ya Trichomonas vaginalis. Wanawake huwa wanapata maambukizi ukeni wakati wanaume wenyewe huwa wanapata maambukizi kwenye tundu la mkojo. Unapataje maambukizi Unaweza kuambukizwa ugonjwa wa TRICHOMONIASIS kwa kushiriki ngono na mtu mwenye maambukizi. Maambukizi wakati wa ujauzito, yanaweza kusababisha mama kujifungua kabla ya wakati au kujifungua mtoto mwenye uzito mdogo. Dalili zake Ugonjwa huu unaweza kusababisha mwanamke kutoa uchafu kama povu wenye rangi ya njano unaoelekea kwenye rangi ya kijani. Uchafu huo mara nyingi huwa na harufu mbaya. Dalili nyingine ni pamoja na maumivu wakati wa tendo la ndoa, maumivu wakati wa kukojoa, kuwashwa sehemu za siri, na wakati mwingine inaweza kusababisha maumivu chini ya kitovu. Kwa wanaume dalili kubwa ni kuhisi muwasho kwenye tundu la mkojo pamoja na maumivu na muwasho baada ya kukojoa. Matibabu Baada ya mwanamke kugundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huu ataandikiwa antibiotiki. Hakikisha umemaliza dawa kabla ya kukutana na mwenzi wako. Ugonjwa wa Malengelenge Ugonjwa wa Malengelenge ni ugonjwa wa ngono unaosababishwa na virusi wanaoitwa Human Simplex Virus. Mtu yeyote anaweza kupata maambukizi. Dalili zinaweza kujitokeza sehemu yoyote ya mwili kuanzia ukeni, kwenye midomo, kwenye njia ya haja kubwa na kwa wanaume kwenye uume. Vile vipele ambavyo huwa vinatokea kwenye midomo maarufu kama vipele vya homa pia vinasababishwa na aina hii ya virusi. Unapataje maambukizi Unaweza kupata maambukizi kwa kufanya ngono kwa njia ya mdomo, ya uke au kwa njia ya haja kubwa na mtu mwenye maambukizi. Unaweza kupata maambukizi hata kama mwezi wako haonyeshi dalili zozote. Pia unaweza kumuambukiza mwenzi wako hata kama na wewe pia hauna dalili Mtoto anaweza kupata maambukizi wakati akiwa tumboni, wakati wa kuzaliwa na baada ya kuzaliwa. Mtoto mchanga huwa anapata maambukizi makali, na unaweza kusababisha mtoto kupoteza maisha.

Dalili zake zikoje. Dalili kubwa ni vipele kama umeungua na maji ya moto. Vipele hivi huwa vina maumivu makali. Vipele vinaweza kutokea sehemu yoyote ya mwili kuanzia kwenye uke, mdomoni, kwenye njia ya haja kubwa, kwenye ngozi na kwenye uume kwa wanaume. Kwa kiasi kikubwa, watu wanaoambukiza ugonjwa wa Malengelenge huwa hawajui kama wana maambukizi au huwa hawana dalili zozote wakati wanapoambukiza wengine. Uchunguzi Mara nyingi daktari anaweza kujua kama una umwa ugonjwa wa Malengelenge kwa kutazama vipele na maelezo ya mgonjwa. Katika nchi zilizoendelea kuna vipimo vya kisasa kwa ajili ya kuchunguza ugonjwa huu. Matibabu Malengelenge ni ugonjwa sugu. Unaweza kujirudia mara kwa mara. Lengo kuu la matibabu ni kupunguza dalili na kupunguza hatari mtu mwenye ugonjwa huu kumuambukiza mwenzi wake. Daktari atamuandikia mgonjwa dawa za kutibu ugonjwa. Baadhi ya wagonjwa wanaweza kuhitaji kutumia dawa kila siku. Matumizi ya kondomu yanasaidia sana kupunguza maambukizi kutoka kwa mwanaume kwenda kwa mwanamke. Lakini matumizi ya kondomu hayasaidii sana kupunguza maambukizi kutoka kwa mwanamke kwenda kwa mwanaume. Iwapo una maambukizi haya wakati wa ujauzito ongea na daktari akuanzishie matibabu kwa sababu ugonjwa huu unaweza kusababisha madhara kwa mtoto.

Maambukizi ya Fungus Maambukizi ya fangasi ukeni mara nyingi huwa yanasababishwa na fangasi wanaojulikana kama Candida albicans. Dalili za fangasi Mwanamke mwenye maambukizi ya fangasi ukeni anaweza kuwa dalili zifuatazo:- maumivu wakati wa kukojoa, muwasho, kuvimba na wekundu pamoja na kutoka uchafu mzito ukeni. Sasa utumie dawa kwa muda gani inategemea na unapata maambukizi ya fangasi mara ngapi kwa mwaka.

▪️Kama unapata maambukizi ya fangasi si zaidi ya mara mbili kwa mwaka na hauna

ugonjwa wowote mwingine. -Hapa unahitaji kutumia dawa za kupaka au za kuingiza ukeni kwa muda wa siku 7 hadi 14. Kwa zile dawa zenye nguvu unatumia kwa muda wa siku 3.

▪️Kama una pata maambukizi zaidi ya mara kwa mwaka yaani mara yanajirudia mara kwa mara. Hapa utaandikiwa dawa za kumeza ambazo utazitumia kwa wiki mara yaani siku ya 1, siku ya 4 na siku ya 7. Baada ya hapo utaandikiwa dawa nyingine za kutumia kila wiki mara 1 kwa muda wa miezi. Au unaweza kuandikiwa dawa za kupaka mara kwa mara.

▪️Kwa kawaida mwanaume haitaji kutibiwa kwa sababu fangasi haziambukizwi kwa njia ya ngono, isipokuwa wale wanaume ambao wana maambukizi ya fangasi kwenye uume.

▪️Kama umenunua dawa mwenyewe, na dalili zikaendelea baada ya kutumia dawa, muone daktari. Wakati mwingine wanawake wengi wanajitibu wenyewe wakifikiri wana fangasi kumbe wana maambukizi mengine.

Maambukizi ya fungus huwa yanatokea mara kwa mara wakati wa ujauzito. Katika kipindi hicho mama mjamzito anashauriwa kutumia dawa za fangasi za kupaka kwa muda wa siku 7. Dawa za kumeza hazishauriwi kutumika wakati wa ujauzito, kwa mfano kutumia kidonge kimoja tu cha Fluconazole kinaweza kusababisha mimba kutoka au mtoto kuzaliwa na kasoro za kimaumbile. Maziwa mgando na maziwa kwa ujumla yana faida nyingi kiafya na unashauriwa uwe unakunywa mara kwa mara. Inawezekana umewahi kusikia unywe maziwa mgando au upake kama tiba ya fangasi za ukeni. Kwa ujumla matumizi ya mtindi pamoja na bidhaa nyingine au supplements zenye probiotics zenye bakteria wa lactobacilli (hawa ndio bakteria wanaopatikana kwenye maziwa mtindi, sasa wanauzwa kabisa kama supplement) hazijathibitishwa kutibu maambukizi ya fangasi ukeni. Kwa hiyo kunywa maziwa na bidhaa nyingine ni tabia nzuri kwa ajili ya kuimarisha afya yako.

Maambukizi kwenye njia ya Mkojo Maambukizi kwenye njia ya mkojo  (UTI ) ni maradhi  ambayo huathiri mfumo wa mkojo yaani  figo, mirija  ya mkojo pamoja  na kibofu  cha mkojo. Kutokana na asili ya maumbile yao, kawaida wanawake huwa wako kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi ya mkojo kuliko wanaume. Maradhi  haya  husababisha  na vimelea wa aina  mbalimbali . Bacteria ndio husababisha  UTI mara nyingi  zaidi  kuliko  vimelea  wengine.  Hata  hivyo fangasi  pia huweza  kusababisha  maambukizi kwenye njia ya mkojo. Unapataje maambukizi kwenye njia ya mkojo. Vimelea  hawa  huweza  kuingia  kwenye njia ya mkojo kwa  njia  mbalimbali. Mojawapo ni kutoka kwenye njia ya  haja kubwa kwenda kwenye njia ya  mkojo hasa wakati wa  kutawaza.Pia  vimelea  hawa  huweza  kuenezwa wakati wa  tendo la ndoa,na pia  kutawaza kwa wanawake huongeza hatari ya kupata maambukizi kwenye njia ya mkojo mara kwa mara. Hata hivyo ugonjwa huu sio ugonjwa wa ngono.

Dalili za  UTI Iwapo  unapata  dalili  hizi  ni dhahiri kuwa  unaweza kuwa  na UTI. •Kuhisi  maumivu  kama  kuungua  wakati wa kukojoa

•Kuhisi  haja  ya kutaka  kukojoa  mara kwa mara na unapokwenda  unapata  mkojo  kiduchu. •Kuhisi  maumivu  chini ya tumbo  na hata  mgongoni •kupata  mkojo wenye  rangi au damu •Uchovu •Kuhisi  homa  au baridi

Vipimo Vipimo  hutolewa  katika  mkojo.  Mkojo unaweza  kufanyiwa  uchunguzi wa moja kwa moja  au kuoteshwa kwa siku kadhaa.

Matibabu Maambukizi ya kibofu cha  mkojo  hayana madhara  makubwa  kama yakitibiwa haraka. Mgonjwa huweza  kuandikiwa dawa  za  kunywa  au sindano  kutegemea hali ya mgonjwa.

Maambukizi  ya figo  huweza  kusababisha mgonjwa kupata  maradhi sugu ya figo  na hivyo  figo  kushindwa  kufanya  kazi vizuri. Pia bacteria  huweza  kuenea katika sehemu  mbalimbali za mwili hivyo kusababisha  madhara zaidi  na hata  kifo.

Unashauriwa  kufanya  yafuatayo ili kupunguza kupata  maambukizi  mara  kwa mara •Hakikisha  unakunywa maji ya kutosha kila siku  angalau  lita 3 •Hakikisha  unakojoa  unapohisi mkojo.  Epuka  kubana  mkojo. •Kojoa  kila  baada ya  tendo la ndoa •Nawa  kabla ya  kukutana  kimwili •Tawaza  toka  mbele  kurudi nyuma kila  baada ya  haja  kubwa •Kula  matunda na vyakula vya protein

Ugonjwa wa Bakteria ukeni (BV) Bacterial Vaginosis ni ugonjwa unaosababishwa na kupungua kwa bakteria rafiki ukeni, na matokeo bakteria ambao sio rafiki wanazaliana kwa wingi na kusababisha dalili. Kwa kawaida ukeni kuna bakteria wengi aina ya Lactobacilli, bakteria hawa huwa wanafanya uke uwe na hali ya asidi. Wanawake wenye ugonjwa huu huwa wana upungufu wa bakteria rafiki na matokeo yake bakteria kama vile G. vaginalis, Prevotella na aina nyingine huwa

wanazaliana kwa wingi. Bacterial Vaginosis ndio ugonjwa unaongoza kusababisha wanawake kutoka uchafu ukeni. Mambo yafuatayo yanaongeza uwezekano wa kupata maambukizi ya BV Kuwa na wapenzi wengi Kuwa kwenye mahusiano ya kingono yenye wapenzi wengi Kutotumia kondomu Kuwa na mpenzi mpya Kutawaza Maambukizi ya Malengelenge Wanawake ambao wapenzi wao wametahiriwa huwa wana uwezekano mdogo wa kupata ugonjwa wa BV. Pia maambukizi ya bakteria huwa yanayoengezeka wakati wa hedhi. Tafiti zinaonyesha kwamba wanawake ambao wanatumia kitanzi cha Shaba wana uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya BV. Matumizi ya njia za homoni za kuzuia mimba yanasaidia kupunguza hatari ya kupata maambukizi ya bakteria ukeni. Dalili za Ugonjwa Zaidi ya nusu ya wagonjwa (50-75%) ya wanawake wenye ugonjwa wa BV huwa hawana dalili. Wanawake wenye dalili huwa wanatoka uchafu ukeni na/au harufu ukeni. Uchafu unaotoka huwa na rangi nyeupe, mwepesi; harufu yake huwa ni "harufu kama shombo ya samaki" ambayo mara nyingi huwa inasikika zaidi baada ya kujamiiana na wakati wa hedhi. Ugonjwa huu kwa kawaida hausababishi muwasho, maumivu au uvimbe ukeni. Iwapo una dalili hizi huwa inaashiria kwamba una maambukizi mengine zaidi.

Madhara ya BV Wanawake wenye ugonjwa wa BV wako katika hatari kubwa ya kuugua magonjwa ya zinaa kama vile VVU, Kisonono, Klamidia, Trichomonas, Masundosu download, na Malengelenge Unaongeza hatari ya kupata maambukizi baada ya kufanyiwa upasuaji wa uzazi Pia BV inaongeza uwezekano wa mwanamke kumuambukiza mpenzi wake ugonjwa wa VVU kwa urahisi zaidi. Ugonjwa wa BV unaongeza hatari ya mimba kuharibika. Wanawake wenye maambukizi haya wako kwenye hatari kubwa ya kujifungua kabla ya wakati Ugonjwa huu unaongeza hatari ya kupata kansa ya shingo ya kizazi. Uchunguzi Madaktari huwa wanatumia vigezo maalumu katika uchunguzi wa ugonjwa huu. Vigezo hivyo vinahusisha aina ya uchafu, harufu ya shombo na kiwa o cha pH ukeni. Kansa ya Shingo ya Kizazi Takwimu zinaonyesha kwamba, mwaka 2020, wagonjwa wapya waliogundulika kuwa na Kansa ya Shingo ya Kizazi walikuwa ni watu 604,000 na watu 342,000 walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huu kote ulimwenguni. Ulimwenguni kote, kansa ya shingo ya kizazi ni

ya nne kusababisha vifo miongoni mwa wanawake. Idadi kubwa ya wagonjwa (84%) wenye saratani ya shingo ya kizazi waligundulika katika maeneo yenye kipato kidogo. Katika nchi zenye kipato kidogo, saratani ya shingo ya kizazi ni ya pili miongoni mwa saratani zinazoathiri wanawake wengi na ni ya tatu kusababisha vifo. Katika bara la Afrika ikiwemo Afrika Mashariki na Afrika ya Kati na Amerika ya Kati, saratani ya shingo ya kizazi ndiyo inayoongoza kwa vifo vinavyohusiana na saratani miongoni mwa wanawake; na bado tafiti mpya zinaonyesha kwamba matukio ya saratani ya shingo ya kizazi yamekuwa yakiongezeka katika baadhi ya maeneo ya Afrika tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000. Ni nini kinachosababisha Kansa ya Shingo ya Kizazi Karibu matukio yote ya saratani ya shingo ya kizazi inatokana na maambukizi ya virusi vinavyojulikana kwa jina la kitaalamu kama human papillomavirus (HPV). Mambo yafuatayo yanaongeza hatari ya kupata kansa ya shingo ya kizazi inayosababishwa na virusi vya HPV:●Kuanza ngono mapema Hatari ya kupata kansa ya kizazi ni kubwa kama mwanamke alianza ngono kwa mara ya kwanza katika umri mdogo. Mwanamke aliyeanza ngono kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa kati ya miaka 18 hadi 20 hatari ya kupata kansa hii ni mara 1.5 zaidi ukilinganisha na yule aliyeanza ngono akiwa na umri wa miaka 21. Mwanamke aliyeanza ngono akiwa na umri chini ya miaka 18 hatari ya kupata kansa ya shingo ya kizazi ni mara mbili zaidi kuliko yule aliye anza akiwa na umri wa miaka 21. ● Kuwa na wapenzi wengi unaofanya nao ngono Ukilinganisha na mwanamke mwenye mwenzi mmoja, hatari ya kupata kansa ya shingo ya kizazi ni karibu mara mbili zaidi kwa mwanamke mwenye wapenzi wawili na mara tatu zaidi kwa yule mwanamke ambaye ana wapenzi sita au zaidi. ● Kuwa na mpenzi mwenye wapenzi wengi au ana maambukizi ya virusi vya HPV. ●Kama umewahi kuugua magonjwa ya ngono (kwa mfano, Klamidia, malengelenge sehemu za siri). ● Kuzaa mapema mtoto wa kwanza (ukiwa na umri wa chini ya miaka 20) na kuzaa mara nyingi (kuzaa mara tatu au zaidi); hii ni kutokana kuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi vya HPV wakati wa kujamiiana ● Kama umewahi kuugua kansa ya uke, mara nyingi maambukizi ya HPV ndiyo chanzo cha matukio mengi ya hali hii). ●Kuwa na ugonjwa unaosababisha Kinga ya mwili kushuka (kwa mfano, maambukizi ya VVU). Matukio ya kansa ambayo hayasababishwi na maambukizi ya virusi vya HPV Ingawa tumeona kwamba karibu matukio yote ya wanawake wenye saratani ya shingo ya kizazi huwa wana maambukizi ya virusi vya HPV, bado kuna matukio mengine ya saratani hii hayasababishwi na virusi hivyo. Zifuatazo ni baadhi ya sababu nyingine zinazoweza kukuweka katika ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.

1. Hali ya dunia ya kijamii na kiuchumi Wanawake wanaoishi katika mazingira yenye umaskini wako katika hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi ukilinganisha na wenzao wanaoishi katika mazingira yenye kipato kikubwa. Hali hii inatokana na wanawake wanaoishi katika mazingira yenye kipato kidogo kuwa na uwezekano mdogo wa kupata huduma za afya na uchunguzi. 2. Matumizi ya muda mrefu ya vidonge vya majira. Tafiti zinaonyesha kwamba wanawake wanaotumia kwa muda mrefu vidonge vya majira (kwa muda wa kuanzia miaka 5 na zaidi) wako katika hatari kubwa ya kupata kansa ya shingo ya kizazi ukilinganisha na wenzao ambao hawakutumia kwa muda mrefu. Hatari huwa inapungua baada ya mwanamke kuacha kutumia vidonge vya majira na baada ya miaka 10 au zaidi hatari inakuwa imekwisha kabisa anakuwa na hatari sawa na wanawake ambao hawakuwahi kutumia 3. Uvutaji sigara. Kuvuta sigara kuna ongeza hatari ya kupata kansa ya shingo ya kizazi kwa zaidi ya asilimia 50. Pia uvutaji wa sigara unasababisha matatizo mengi ya kiafya. Ni wakati wa kuacha na kumshawishi mwenzi wako kuacha kuvuta sigara. 4. Inaweza kurithiwa. Zamani wataalamu walikuwa wanafikiria kwamba pengine kansa ya shingo ya kizazi kwa wanafamilia inaweza kusababishwa na kuambukizana virusi vya HPV, lakini kwa sasa tafiti zinaonyesha kwamba kuna uwezekano mkubwa kansa ya shingo ya kizazi inaweza kurithiwa. 5. Una hatari ndogo ya kupata kansa ya shingo ya kizazi kama mumeo ametahiriwa. Wanawake ambao wenzi wao wametahiriwa huwa wana hatari ndogo ya kuugua ugonjwa wa kansa ya shingo ya kizazi. Dalili za Saratani ya Shingo ya Kizazi Mara nyingi katika hatua za mwanzo kansa ya shingo ya kizazi huwa haina dalili, hii ndio sababu kubwa kwa nini wanawake wote wanasisitizwa kwenda hospitali ili kufanyiwa uchunguzi. Kwa wagonjwa wasiokuwa na dalili, Saratani ya shingo ya kizazi inaweza kugundulika kwa bahati tu wakati wa kipimo cha uchunguzi au wakati daktari anampima mwanamke njia wakati wa uchaguzi wa kawaida wa matatizo mengine ya kiafya. Kwa wale walio na dalili, mara nyingi hizi zifuatazo ndio dalili ambazo huwa zinajitokeza]: ●Kutokwa na damu nyingi ukeni au damu kutoka bila mpangilio. ●Kutokwa na damu baada ya tendo la ndoa (mara nyingi mwanaume anaona damu kwenye uume wake baada ya tendo) Baadhi ya wagonjwa huwa wanatoka uchafu ukeni ambao unaweza kuwa kama majimaji, ute, au usaha wenye harufu mbaya. Hali hii inaweza kuchanganywa na magonjwa maambukizi ya kawaida ya uke. Vipimo na uchunguzi

Kwa kawaida mwanamke anagundulika kama ana kansa ya shingo ya kizazi kwa kuchukuliwa kipande cha nyama kwenye shingo ya kizazi na kupelekwa kufanyiwa uchunguzi maabara. Matibabu. Matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi inategemea na hatua ya ugonjwa. Hata hivyo matibabu yanaweza kujumuisha upasuaji, mionzi na dawa za saratani. Uchunguzi wa Kawaida wa afya Kwa sababu katika hatua za awali za ugonjwa huwa hauonyeshi dalili, inapendekezwa kwamba kila mwanamke awe anafanyiwa uchunguzi mara kwa mara. Uchunguzi ukifanywa mara kwa mara inasaidia kugundua ugonjwa ukiwa katika hatua za awali. Yafuatayo ni mapendekezo ya wakati gani ufanye uchunguzi kulingana na umri wako:Wanawake wenye umri wa kati ya miaka 21 hadi 29 Kwa wale wanawake ambao hawana hatari kubwa (mfano hawana VVU au ugonjwa mwingine wowote unaoshusha kinga ya mwili) wanashauriwa kufanya kipimo cha uchunguzi cha Pap Smear kila baada ya miaka 3. Kwenye yale maeneo ambako kuna vipimo vya kupima Virusi vya HPV unaweza kuanza ukiwa na umri wa miaka 25 na kufanyiwa kipimo kila baada ya miaka 5. Hata hivyo kipimo cha namna hii hakipatikani katika maeneo mengi. Wanawake wenye umri wa kati ya miaka 30 hadi 65. Kwa wanawake wenye umri huu wanaweza kufanyiwa uchunguzi kwa kutumia kipimo cha Pap (Pap test) kila baada ya miaka 3. Kama katika eneo lako kuna kipimo cha kupima virus vya HPV unaweza kufanyiwa uchunguzi kwa kutumia vipimo vyote viwili kila baada ya miaka 3. Kwa wale wanawake ambao mfuko wa uzazi pamoja na shingo yake vilitolewa kwa sababu nyingine yoyote tofauti na kansa ya shingo ya kizazi hawahitaji kufanyiwa uchunguzi. Uchunguzi kwa wanawake wenye hatari kubwa ya kupata kansa ya shingo ya kizazi. Wanawake ambao wanaishi na VVU, au wana ugonjwa au hali yoyote inayoshusha kinga ya mwili au mama zao walitumia dawa ya diethylstilbestrol (DES) wakiwa wajawazito wana hatari kubwa zaidi ya kupata kansa ya shingo ya kizazi. Kwa wanawake wanaoishi na VVU, wanapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kwanza wa shingo ya kizazi mara tu anapogundulika kuwa na maambukizi ya VVU lakini isiwe kwa mwanamke mwenye umri wa chini ya miaka 21. Baada ya kipimo cha mwanzo, mwanamke huyo atahitaji kurudia kipimo kila baada ya miezi 12 kwa muda wa miaka 3. Kama kipimo hakitaonyesha ugonjwa au mabadiliko kwenye shingo ya kizazi ataendelea kufanyiwa uchunguzi kila baada ya miaka 3. Mambo ya kufanya Kupunguza Hatari ya Kupata Kansa ya Shingo ya Kizazi Chanjo

Inapendekezwa watoto wote wa kike wenye umri wa kati ya miaka 9 hadi 13 wapate chanjo ya HPV. Acha kuvuta sigara. Uvutaji Sigara unaongeza hatari ya kupata Kansa ya Shingo ya Kizazi. Kama wewe unavuta acha na mshauri mwenzi wako aache. Watoto wa kiume watahiriwe na mshauri mwenzi wako atahiriwe pia. Wanawake ambao waume zao wametahiriwa wana hatari ndogo ya kuugua saratani ya shingo ya kizazi. Tumia kondom Matumizi ya kondomu yatakuepusha na maambukizi ya virusi vya HPV pamoja na magonjwa mengine ya ngono. Fanya uchunguzi Iwapo utashindwa kabisa kufanya uchunguzi kama ilivyo elezwa hapo juu, ni muhimu sana kufanya uchunguzi unpokuwa na umri wa kati ya miaka 30 hadi 49. Watoto wapate Elimu ya afya Ni muhimu watoto wote wa kike na wa kiume wakipita elimu ya afya juu ya magonjwa mbalimbali ikiwemo elimu ya maambukizi ya virusi vya HPV na jinsi ya kujikinga.